NAIBU Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko amesema adhma ya serikali ya Awamu ya Sita ni kufikisha umeme katika kila kitongoji kabla ya uchaguzi wa 2025.
Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akiwasha umeme kwenye Kijiji cha Ndalibo, Kata ya Mtanana Wilaya ya Kongwa sambamba na kuzindua kisima cha maji ambacho kitakuwa kikitumia umeme kwa manufaa ya wananchi wa eneo hilo.
Dkt.Biteko amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia anapambana usiku na mchana kuhakikisha umeme unapatikana na kuinua hali za maisha ya wananchi waliopo vijijini kwani umeme sio anasa bali ni jambo la muhimu kwa sasa.
“Katika sekta ya umeme tutafanya kila kupeleka umeme katika kila kitongoji kupeleka umeme katika kila eneo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025 katika uongozi huu wa serikali ya Awamu ya Sita umeme sio anasa bali ni jambo la lazima.”amesema Dkt.Biteko
Aidha, amewaagiza TANESCO na REA kuhakikisha Vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme kuhakikisha vinawekewa huduma hiyo muhimu kwa haraka
Katika hatua nyingine Biteko amesema serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha nishati ya kupikia kwa kuboresha gharama za gesi na majiko ya kupikia
Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Nishati Vijiji (REA), Mhandisi Thomas Mbaga amesema Mkoa wa Dodoma Una jumla ya vijiji 580 ambapo vijiji 410 sawa na asilimia 70 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi ya REA.
Amesema REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa wa Dodoma lengo ni kuwafikishia huduma bora wananchi ili kuboresha huduma za jamii.
“Kwasasa REA inaendelea na mikakati wa kupeleka umeme katika migodi midogo na maeneo ya kilimo ambayo hayajafikiwa na umeme ambapo katika hatua hii migodi 13 itafikiwa katika wilaya za Mpwapwa, Chamwino,Bahi, Dodoma na Kondoa.








